Virusi vya Ebola vinapoingia mwilini huanzisha mchakato mgumu unaoweza kusababisha madhara makubwa katika mfumo mzima wa mwili.
Kwa miongo kadhaa, ugonjwa wa virusi vya Ebola umekuwa miongoni mwa magonjwa yanayoibua hofu kubwa zaidi duniani. Kila mara mlipuko unaporipotiwa, jamii huingiwa na wasiwasi kutokana na kasi ya ugonjwa huo kuenea na kiwango chake kikubwa cha vifo.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa Ebola si ugonjwa unaosambaa kwa urahisi kama watu wengi wanavyodhani. Tofauti na magonjwa ya mfumo wa upumuaji kama COVID-19, Ebola haisambai kupitia hewa. Maambukizi hutokea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa. Kwa mujibu wa Dkt. Moses Masika, mtaalamu wa virusi, ufahamu sahihi kuhusu ugonjwa huu ni silaha muhimu katika kuzuia maambukizi na kuokoa maisha wakati wa mlipuko.
Ebola ni nini?
Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na kundi la virusi vinavyojulikana kama orthoebolaviruses. Virusi hivi huathiri binadamu pamoja na baadhi ya wanyama, hususan nyani, sokwe na popo wa matunda ambao wanaaminika kuwa miongoni mwa hifadhi asilia za virusi hivyo.
Ugonjwa huo ulitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976 katika eneo ambalo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kulingana na Shirika la Afya Duniani, kiwango cha vifo ni wastani wa asilimia 50, ingawa kimewahi kushuka hadi asilimia 25 au kupanda hadi asilimia 90 kulingana na aina ya virusi, mazingira ya mlipuko na upatikanaji wa huduma za afya.
Dkt. Masika anasema kiwango hicho kikubwa cha vifo ndicho kinachoufanya ugonjwa huu kuogopwa sana. “Kwa wastani, kati ya wagonjwa wawili mmoja anaweza kufariki. Hilo pekee linaonyesha jinsi ugonjwa huu ulivyo hatari. Pia dalili zake zinaweza kuwa za kutisha, hasa pale mgonjwa anapoanza kuvuja damu na viungo vya mwili vinapoanza kushindwa kufanya kazi.”
Ebola huathirije mwili?
Virusi vya Ebola vinapoingia mwilini huanzisha mchakato mgumu unaoweza kusababisha madhara makubwa katika mfumo mzima wa mwili. Virusi hivyo huchochea mfumo wa kinga kwa kiwango kikubwa kupita kawaida. Badala ya kupambana na virusi pekee, mfumo wa kinga huanza kuharibu tishu na viungo vya mwili.
“Mfumo wa kinga huanza kuushambulia mwili wenyewe. Madhara makubwa huonekana kwenye mishipa ya damu. Mishipa inapoharibiwa, damu huanza kuvuja ndani ya mwili na viungo mbalimbali hukosa damu ya kutosha. Hali hiyo inaweza kusababisha kushindwa kwa figo, ini na viungo vingine muhimu,” anaeleza Dkt. Masika.

Ebola husambaa vipi?
Mtu hawezi kuambukizwa Ebola kwa kusimama karibu na mgonjwa au kwa kupumua hewa moja naye. Maambukizi hutokea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa, ikiwemo damu, mate, mkojo, kinyesi, jasho, machozi, manii na maziwa ya mama.
Dkt. Masika anaeleza kuwa majimaji hayo yanaweza pia kuchafua nguo au matandiko. “Majimaji yoyote yanayotoka kwa mtu aliyeambukizwa yanaweza kusababisha maambukizi. Ikiwa yamechafulia nguo, matandiko au sehemu yoyote na mtu mwingine akayagusa, anaweza kuambukizwa.” Wahudumu wa afya, wanafamilia na walezi wanaomhudumia mgonjwa wa Ebola huwa katika hatari kubwa zaidi ikiwa hawatachukua tahadhari zinazohitajika.
Dalili za Ebola
Changamoto kubwa katika kudhibiti Ebola ni kwamba dalili zake za mwanzo zinafanana sana na zile za magonjwa mengi yanayoambatana na homa. Katika hatua za awali, mgonjwa anaweza kuwa na homa, maumivu makali ya kichwa, uchovu, udhaifu mkubwa, maumivu ya misuli, maumivu ya viungo, maumivu ya koo na baridi mwilini.
“Kama hutakuwa na kiwango cha juu cha tahadhari, ni rahisi kuikosa Ebola kwa sababu mwanzoni huonekana kama ugonjwa wa kawaida unaosababisha homa,” anasema Dkt. Masika. Kwa sababu hiyo, historia ya safari za mgonjwa na mawasiliano yake na watu walio katika maeneo yenye mlipuko huwa muhimu sana katika uchunguzi wa awali.
Dalili za Ebola hujitokeza kati ya siku mbili na ishirini na moja baada ya maambukizi, ingawa watu wengi huanza kuonyesha dalili kati ya siku nane hadi kumi. Kadri ugonjwa unavyoendelea, mgonjwa anaweza kutapika, kuharisha, kupata macho mekundu, upele wa ngozi na maumivu ya kifua. Katika hatua kali zaidi, mgonjwa anaweza kutokwa damu puani, kutapika damu, kupata michubuko chini ya ngozi, kuchanganyikiwa kiakili na kushindwa kwa figo au ini.
“Kadri ugonjwa unavyozidi kuwa mbaya, viungo mbalimbali vya mwili huanza kushindwa kufanya kazi. Mgonjwa anaweza kuacha kutoa mkojo kutokana na figo kuathirika. Wengine huanza kuchanganyikiwa au kubadilika kitabia,” anasema Dkt. Masika.
Aina za virusi vya Ebola
Kuna aina sita za virusi vya Ebola zilizotambuliwa na wanasayansi: Zaire, Sudan, Bundibugyo, Tai Forest, Reston na Bombali. Kwa mujibu wa Dkt. Masika, aina tatu za kwanza ndizo zilizosababisha milipuko mingi kwa binadamu.
“Virusi vya Zaire, Sudan na Bundibugyo ndivyo vimesababisha idadi kubwa ya maambukizi. Aina nyingine zimeonekana mara chache sana au zimegunduliwa zaidi kwa wanyama.”
Miongoni mwa aina zinazofuatiliwa kwa karibu ni virusi vya Bundibugyo. Dkt. Masika anasema changamoto kubwa ni kwamba taarifa kuhusu aina hii bado ni chache.
“Hatuna tiba maalum ya Bundibugyo na pia hatuna chanjo maalum dhidi yake. Chanjo zilizopo sasa zimeundwa kwa ajili ya Ebola ya Zaire na hazitoi kinga dhidi ya Bundibugyo.” Hata hivyo, huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Bundibugyo ni sawa na zile zinazotolewa kwa wagonjwa wa aina nyingine za Ebola.
Utambuzi na matibabu
Kwa sababu dalili zake zinafanana na magonjwa mengine, Ebola haiwezi kuthibitishwa kwa kuangalia dalili pekee. Uthibitisho huhitaji vipimo vya maabara, hasa kipimo cha damu cha Polymerase Chain Reaction, ambacho hutambua vinasaba vya virusi mwilini. Wakati wa kusubiri majibu, wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola hutengwa ili kuzuia maambukizi.
Kwa sasa, hakuna tiba ya moja kwa moja kwa baadhi ya aina za Ebola. Hata hivyo, wagonjwa wanaweza kuokolewa kupitia huduma bora za matibabu. Dkt. Masika anasisitiza kuwa ugunduzi wa mapema ndio hatua muhimu zaidi.
“Tunapomgundua mgonjwa mapema, tunaweza kumtenga ili kuwalinda wengine na kuanza kumpatia huduma za kitabibu mara moja.” Huduma hizo ni pamoja na kumpatia maji na virutubisho, kudhibiti maumivu, kusahihisha upungufu wa maji mwilini na kusaidia viungo vinavyoathirika.
Ushirikiano wa jamii
Dkt. Masika anasema ukosefu wa imani kwa mamlaka za afya unaweza kuwafanya watu kuficha wagonjwa au kukataa kwenda hospitalini. “Watu wakikosa imani, wanaweza kuwahudumia wagonjwa nyumbani au kukataa kufanyiwa uchunguzi. Hali hiyo huongeza hatari ya maambukizi kusambaa.” Jamii zinapowaamini wahudumu wa afya, huwa tayari kuripoti visa vinavyoshukiwa na kushirikiana katika kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa.
Anabainisha pia kuwa mtu mwenye Ebola hawezi kuwaambukiza wengine kabla hajaanza kuonyesha dalili. “Endapo hana dalili, hawezi kueneza ugonjwa. Lakini mara tu dalili zinapoanza, anaweza kuambukiza wengine. Hata baada ya kifo, mwili wa marehemu unaweza kuendelea kuwa chanzo cha maambukizi.”
Jinsi ya kujikinga
Maambukizi ya Ebola yanaweza kuzuiwa kwa hatua za msingi: kuzuia kugusana na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa, kuepuka kushughulikia miili ya watu wanaoshukiwa kufariki kutokana na Ebola, kuepuka kugusana na wanyamapori, kutumia vifaa sahihi vya kujikinga na kutafuta huduma za afya mara moja unapopata dalili. Kwa wahudumu wa afya, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga ni muhimu zaidi.
“Ni lazima wahudumu wa afya wapate vifaa vya kujikinga na mafunzo ya namna ya kuvitumia kwa usahihi. Hii inawalinda wao na pia jamii wanazotoka,” anasema Dkt. Masika.
Ebola bado ni moja ya magonjwa hatari zaidi ya kuambukiza duniani, lakini si ugonjwa usioweza kudhibitiwa. Ugunduzi wa mapema, vipimo vya haraka, huduma bora za matibabu na ushirikiano wa jamii vinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo na kusitisha milipuko.
Kwa watu wanaosafiri kwenda maeneo yenye mlipuko, wataalamu wanashauri kujifuatilia kwa siku 21 baada ya kurejea na kutafuta huduma za afya mara moja endapo watapata dalili zozote. Katika vita dhidi ya Ebola, maarifa sahihi, tahadhari na hatua za haraka vinaendelea kuwa silaha muhimu zaidi za kuokoa maisha.








