Mfumo mpya wa bima ya afya nchini Kenya unatambua familia za wake wengi. Hivi ndivyo unavyoweza kuhakikisha kila mmoja analindwa.
Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) imebadilisha huduma za afya nchini Kenya kwa kuanzisha mfumo jumuishi unaotambua miundo tofauti ya familia nchini.
Tofauti na mfumo wa zamani wa NHIF, uliotambua mke mmoja na mume mmoja pekee, sasa SHA inaruhusu usajili wa hadi wake wanne, mume mmoja, na idadi isiyo na kikomo ya watoto, mradi uweze kuthibitisha uhusiano huo.
Akizungumza katika mkutano wa umma tarehe 23 Novemba 2025, Waziri wa Afya Aden Duale alisema:
“NHIF ilikuwa inatambua mke mmoja na mume mmoja tu, lakini SHA inaruhusu hadi wake wanne, mume mmoja na idadi isiyo na kikomo ya watoto, mradi uweze kuthibitisha kuwa hao ni watoto wako.”
Kuongeza wake wengi chini ya sheria ya bima ya Afya ya Jamii (SHI)
Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii ndiyo msingi wa kisheria wa mpango huu.
Kanuni ndogo ya (4) inasema:“Mwenye wake zaidi ya mmoja atalipa mchango kwa kila mke kama itakavyoamuliwa na chombo cha kupima uwezo wa kipato (means testing), na mke huyo atastahili kupata huduma siku kumi na nne baada ya kutangazwa chini ya kanuni ndogo ya (1) na kulipwa kwa mchango.”
Katika mpango huu, anayewalipia wake wengi anapaswa kulipa mchango tofauti kwa kila mke. Kiasi hicho huamuliwa kupitia mfumo wa means testing, unaotathmini kipato cha jumla cha familia.
Kuna muda wa kusubiri wa siku 14 kabla ya mke aliyeongezwa kuanza kupata huduma, ambao ni mfupi kuliko siku 30 kwa wategemezi wengine.
SHA pia hutoa huduma kupitia mpango wa Linda Jamii, unaowahudumia akina mama kuanzia ujauzito, huduma za kabla ya kujifungua, kujifungua, hadi chanjo.
Mahitaji kabla ya usajili
Kabla ya kuongeza wake wengine kwenye akaunti yako ya SHA, hakikisha una yafuatayo:
Kwa kila mke:
- Kitambulisho halali cha Taifa (ID)
- Nambari ya simu inayotumika (kwa uthibitisho wa OTP)
- Usajili binafsi wa SHA (lazima uwe umekamilika kwanza)
Uthibitisho wa ndoa (moja ya hizi):
- Cheti cha ndoa
- Hati ya kiapo cha ndoa
- Barua kutoka kwa chifu wa eneo lako kuthibitisha ndoa
Mchakato wa usajili hatua kwa hatua
Hatua ya 1: Usajili binafsi
Kila mke lazima ajiandikishe kwanza kivyake kupitia tovuti ya Afya Yangu (afyayangu.go.ke) au kwa kupiga *147#, akitumia nambari ya ID na simu yake.
Hatua ya 2: Kuongeza mke kama mtegemezi
Ingia kwenye akaunti yako ya SHA kupitia sha.go.ke au Afya Yangu
Nenda kwenye Maelezo yako (My Profile), kisha ongeza Watengemezi (Dependants)
- Chagua “Mke” (Spouse)
- Ingiza nambari ya ID ya mke wako
- Wasilisha uthibitisho wa ndoa
- Weka nambari ya simu ya mke wako; atapokea OTP kuthibitisha
- Kamilisha na uwasilishe ombi
Hatua ya 3: Subiri uthibitisho
Ombi lako litaangaziwa, na mke wako ataongezwa kwenye usajili wa familia yako baada ya kuidhinishwa.
Nani analipa michango?
Kwa wafanyakazi wanaolipwa mishahara, michango hukatwa moja kwa moja kutoka kwa mshahara wa kila mwenzi anayefanya kazi.
Kwa familia zisizo na mshahara wa kudumu, familia huamua nani atalipa.
Kipato cha jumla cha familia hutumika kuamua kiwango cha mchango.
Kwa kawaida, kuna muda wa kusubiri wa siku 30 kabla ya mke mpya kupata huduma, isipokuwa pale anapochukua nafasi ya mwenzi aliyefariki ambapo muda huo hauhitajiki.
Kwa ndoa za wake wengi, huenda ukahitaji kusajili wake wengine chini ya familia tofauti lakini ukiwaunganisha nawe kama mfadhili mkuu wa malipo, hasa kama umeajiriwa rasmi au uko chini ya hazina ya afya ya watumishi wa umma (POMSF).
Akielezea mpango wa Linda Jamii, Waziri Duale alisema: “Hatuwalindi akina mama pekee au watoto pekee. Tunawahudumia akina mama kuanzia ujauzito, huduma za kabla ya kujifungua, hadi kujifungua na chanjo, ndio maana unaitwa Linda Jamii.”
Ikiwa mtegemezi atafariki, julisha SHA mara moja kwa kuwasilisha stakabadhi za uthibitisho wa kifo.
Kwa msaada zaidi, tembelea ofisi yoyote ya SHA, Huduma Centre, hospitali ya umma yenye dawati la SHA, au piga *147#.





