Wakenya wanaweza kuwasilisha malipo ya SHA kwa awamu ndogo za kila siku, kila wiki au kila mwezi kwa gharama nafuu.
Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) imeanzisha njia rahisi, nafuu na jumuishi kwa Wakenya kuwasilisha malipo yao ya kila mwaka ya afya.
Mpango huu unaojulikana kama Lipa SHA Pole Pole au Lipa Mos Mos. Unawawezesha watu nchini Kenya kuwasilisha malipo ya SHA kwa awamu ndogo za kila siku, kila wiki au kila mwezi ili kuhakikisha hakuna familia inayosalia nyuma katika kupata huduma za afya.
Kwa kuruhusu malipo madogo lakini ya mara kwa mara, Lipa SHA Pole Pole inawasaidia Wakenya kudumisha bima ya afya bila kuathiri sana hali yao ya kifedha, huku ikiimarisha uendelevu wa hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).
Lipa SHA Pole Pole ni ushirikiano wa kimkakati kati ya Wizara ya Afya, Wizara ya Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs), makampuni ya mawasiliano ya simu, taasisi za kifedha na hazina ya Hustler. Mfumo huu umetajwa kuwa rahisi, unaotumia simu, na rafiki kwa mtumiaji ili kila raia anayestahili aweze kuutumia bila vikwazo.
Jinsi ya kuanza kutumia Lipa SHA Pole Pole
Mtu yeyote mwenye simu ya rununu anaweza kujisajili kwa SHA na kuanza kuchangia mara moja. Huu hapa mwongozo wa hatua kwa hatua:
- Piga *147# kwenye simu yako.
- Menyu itajitokeza. Chagua kundi lako:
- Raia wa Kenya
- Mkazi wa Kigeni
- Mkimbizi
- Ikiwa wewe ni raia wa Kenya, chagua 1.
- Weka nambari yako ya Kitambulisho cha Taifa (ID) utakapoagizwa.
- Chagua 2: Wasilisha malipo
- Chagua njia ya malipo unayopendelea:
- Jilipie (Pay for Self)
- Lipa Pole Pole
- Mlipie mtu mwingine (Pay for Other)
- Ukichagua Lipa Pole Pole, menyu nyingine itatokea ikikuomba:
- Uchague mfadhili wa malipo. Chagua:
- Hustler Fund
- Mwisho, chagua mpango wa malipo unaokufaa:
- Kila siku
- Kila wiki
- Kila mwezi
Kufikia Mei 2025, zaidi ya Wakenya milioni 22 walikuwa wamejisajili chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, zikionyesha kuwa mifumo ya kidijitali ya SHA sasa iko imara kikamilifu na inawezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi kote nchini.
Serikali ilibainisha kuwa Wakenya milioni 1.2 walikuwa wamehudumiwa kwa madai yaliyofikia takriban shilingi bilioni 45.
Kwa kuwa Wakenya wengi hufanya kazi katika sekta zisizo rasmi au hutegemea kipato kisicho cha uhakika, Lipa SHA Pole Pole inatoa njia ya haki na halisi ya kuendelea kulindwa kiafya bila kulazimika kulipa pesa nyingi mara moja.
Kwa watu wanaojiajiri, SHA huruhusu malipo rahisi kupitia M-Pesa na majukwaa mengine ya pesa za simu, uhamisho wa benki, au katika vituo vilivyoidhinishwa. Mtu anaweza pia kujiandikisha na kusimamia malipo yake kupitia tovuti ya SHA au kwenye vituo vya huduma kama Huduma Centres na hospitali zilizoteuliwa.
SHA hutumia mfumo wa kupima uwezo wa kipato (Means Testing) kwa familia zisizo na kipato cha kudumu. Ili kuutumia:
- Tembelea afyayangu.go.ke
- Ingia na uende kwenye “Maelezo Yangu”(My Profile)
- Chini ya “Mapato”(Income), chagua “Umejiajiri”(Self-employed)
- Jibu maswali yanayoangaziwa chini ya mpango wa kupima uwezo wa kipato(Means Testing)
Kiasi cha malipo yako kitahesabiwa kulingana na ukubwa wa familia yako, hali ya makazi, kiwango cha elimu, na kipato chako. SHA itapendekeza kiasi cha kulipa kila mwezi au kila mwaka kulingana na uwezo wako.
Jinsi ya kulipa
1. Kupitia Paybill ya M-Pesa
- Nenda kwenye Lipa na M-Pesa
- Chagua Paybill
- Nambari ya Paybill: 200222
- Nambari ya akaunti: Nambari yako ya Kitambulisho cha Taifa (ID)
- Weka kiasi cha pesa na PIN ya M-Pesa kuthibitisha
2. Kupitia njia ya USSD
- Piga *147#
- Weka nambari yako ya ID
- Chagua Lipa (Make Payment) na ufuate maelekezo
3. Kupitia tovuti
- Tembelea afyayangu.go.ke
- Ingia na uende kwenye sehemu ya malipo (payment section)
- Fuata hatua zilizoonyeshwa ili kulipa mtandaoni
Mambo muhimu ya kukumbuka
- Hakikisha nambari yako ya ID ni sahihi kabla ya kufanya malipo.
- Baada ya kulipa, hakiki akaunti yako ya SHA ili kuhakikisha malipo yako yamefanikishwa.
- Kwa usaidizi, tembelea kituo chochote cha SHA, piga simu kwa huduma kwa wateja, au tembelea tovuti rasmi kwa maelezo zaidi.





